SIKU YA KATIBA

Tarehe hii, miaka kumi iliyopita, Wakenya walishuhudia tukio la kihistoria. Rais Kibaki, katika bustani ya Uhuru, alitia sahihi yake na hivyo rasimisha katiba mpya. Katiba ya Kenya, 2010. Aliinua stakabadhi hiyo na kuonyesha maelfu ya Wakenya waliohudhuria hafla hiyo muhimu. Alipokezwa kwa shangwe na nderemo. Ramsa ya Wakenya ilikuwa dhahiri.

PICHA: NATION.CO.KE

Kurasimishwa kwa Katiba ya Kenya, 2010, kulikuwa tokeo la misururu ya matukio ya kisiasa. Matukio ambayo yalianza pindi tu baada ya Wakenya kuchukua uhuru wao kutoka kwa wakoloni, Waiingereza. Yakini, imekuwa miaka iliyofumwa kwa vuta nikuvute baina ya serikali na wanaharakati. Ramramu ya Wakenya wamevunjwa mbavu na polisi, kutiwa gerezani bila kusikizwa kortini, kutorokea nchi zingine kwa kuhofia maisha yao, na wengine kufa katika harakati hiyo. Harakati ya kupigania mfumo mpya wa sheria.

PICHA: TUKO. CO. KE

Kilele cha rangaito hii ilikuwa rabsha za 2007/2008. Maelfu ya Wakenya walipoteza maisha yao. Wakenya wengi zaidi walipoteza nyumba na biashara zao. Miaka kumi na mitatu baadaye, bado matukio hayo ni tenge tahanani. Rabsha za 2007/2008 zilikuwa taashira kwamba hali sio hali. Kwamba tahabibu ya mawimbi hayadhibitiki. Kwamba tusipobadili mkondo chombo chetu kitaangamia.

PICHA: KITUOCHASHERIA

Katiba ya Kenya, 2010 basi, ilikuwa huo mkondo mpya. Ilikuwa maafikiano kati ya nahodha na wanabaharia kuokoa chombo chao. Waama, ilikuwa muda wa kukubali busara ya wahenga. Kwamba, mwana wa Kwale kufa maji mazoea.

Katiba ya Kenya, 2010 imesifiwa kuwa katiba endelezi. Tofauti na katiba ya hapo awali, Katiba hii imechukua mamlaka za rais na kuzigawanya kwa ngazi mbalimbali za uongozi. Kipengele chake kikuu ni ugatuzi. Isitoshe, imetengeneza Seneti kuwa chumba kingine cha bunge. Haya ni baadhi tu ya mambo mengi yaliyoletwa na Katiba ya Kenya, 2010.

PICHA: PD. CO. KE

Miaka kumi baadaye, ni muda wa kutafakari na kutafakuri kuhusu vipengele mbalimbai vya Katiba yetu. Je, vyeo vipya vya maseneta, wakilishi wa wanawake na wajumbe, vimetufaa? Je, uhuru wa vitengo vikuu vya serikali umetaadhimishwa? Je, Sura ya Nne; Mswaada ya Haki na Sura ya Sita; Uongozi na Uadilifu, zimefuatwa?

Je, Katiba ya Kenya, 2010 imetufaa? Kama jibu ni ‘ndio’, basi swali ni; tunaweza kuboresha utekelezaji wake kwa njia zipi? Kama jibu ni ‘hapana’, basi swali ni; ni hatua zipi tunaweza kuchukua kurekebisha mkondo huu?

Je, huwa unasoma Katiba ama wewe ni mojawapo wa wale ambao unaamini kuwa Katiba iliundiwa wanasheria? Unafahamu sheria zinazotumika kukuongoza? Je, unajua haki zako? 

Swali kwako, Mkenya!

15,220 thoughts on “SIKU YA KATIBA